Migomo na maandamano yaongezeka Sudan, sasa ni zamu ya madaktari, wauguzi
Madaktari nchini Sudan wameojiunga na matabaka mbalimbali ya nchi hiyo kupinga sera za serikali ya Rais Omar al Bashir na mwenendo wake wa kupuuza matakwa ya kisheria ya tabaka hilo.
Ripoti zinasema madaktari na wauguzi wa Sudan jana walianza mgomo wa Siku tatu kuishinikiza serikali ya nchi hiyo ili ikubali matakwa yao. Madaktari wasiopungua 12 wametiwa nguvuni katika mgomo na maandamano hayo.
Jumuiya ya Madaktari ya Sudan imetangaza kuwa, mgomo na maandamano hayo yanafanyika kupinga tabia ya askari usalama kuwatia nguvuni ovyo madaktari na wauguzi, kuamiliana vibaya na vituo vya afya na tiba na vilevile kupuuzwa matakwa ya kisheria ya tabaka hilo.
Migomo na maandamano ya madaktari nchini Sudan yanafuatia machafuko na maandamano yanayoendelea katika pembe mbalimbali za nchi hiyo kupinga hali mbaya ya kijamii na kiuchumi na sera za serikali ya Rais Omar al Bashir. Maandamano hayo yameshika kasi zaidi baada ya serikali ya Khartoum kufuta ruzuku ya wananchi katika sekta ya nishati, suala ambalo limesababisha kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu na ughali mkubwa wa maisha.