Mke wa Mugabe asema yeye ndiye rais wa Zimbambwe
Mke wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amesema yeye ndiye rais wa nchi hiyo kwa kuwa anatekeleza majukumu yote ya urais pamoja na mumewe.
Grace Mugabe amekiambia kikao cha Tawi la Wanawake la chama tawala ZANU-PF kuwa, hana haja ya kugombea wadhifa wa Makamu wa Rais kwa kuwa tayari anaendesha shughuli za kila siku za ofisi ya rais.
Matamshi ya mke wa rais wa Zimbabwe yamezusha manung'uniko kutoka kwa makada wa ngazi za juu wa chama tawala, ambao awali walikuwa wameeleza kutoridhia mpango wa kukifanya kiti cha rais kuwa cha kifamilia.
Hii ni katika hali ambayo, licha ya maandamano na malalamiko ya nchi dhidi ya serikali, lakini Rais Mugabe ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 36 na ambaye ana umri wa miaka 92 hivi karibuni aliwaahidi wafuasi wake kuwa atagombea tena uchaguzi wa rais ujao uliopangwa kufanyika mwaka 2018.
Mbali na Grace Mugabe, wanasiasa wengine waliotazamiwa kurithi kiti cha Rais Mugabe kupitia chama tawala ZANU-PF ni makamu wake wawili Phelekezela Mphoko na Emmerson Mnangagwa.
Katika siku za hivi karibuni, Zimbabwe imekuwa ikishuhudia maandamano ya wapinzani wanaomtaka Rais Mugabe aondoke madarakani wakisisitiza kuwa ameshindwa kutatua matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa ajira nchini humo.