Madaktari wasimamisha mgomo wao nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20038-madaktari_wasimamisha_mgomo_wao_nchini_sudan
Mgomo wa nchi nzima wa madaktari huko Sudan umesitishwa kwa muda baada ya vyombo vya dola kuwaachilia huru madaktari wawili waliokuwa wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kushiriki katika mgomo wa kuipinga serikali.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Nov 23, 2016 11:33 UTC
  • Madaktari wasimamisha mgomo wao nchini Sudan

Mgomo wa nchi nzima wa madaktari huko Sudan umesitishwa kwa muda baada ya vyombo vya dola kuwaachilia huru madaktari wawili waliokuwa wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kushiriki katika mgomo wa kuipinga serikali.

Shirika la habari la IRNA limeinukuu Kamati Kuu ya Jumuiya ya Madaktari nchini Sudan ikisema leo kuwa, vyombo vya dola vimewaachilia huru madaktari 11 waliokuwa wamewekwa kizuizini na  kwamba hivi sasa amebakia daktari mmoja tu mikononi mwa vyombo hivyo.

Kabla ya hapo, askari wa serikali ya Sudan walivamia nyumba ya daktari mmoja na kumtia mbaroni na kumpeleka kusikojulikana kwa tuhuma za kushiriki katika mgomo dhidi ya serikali.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hatua ya vyombo vya dola nchini Sudan ya kuwaachilia huru madaktari hao imechukuliwa baada ya kamati kuu ya jumuiya ya madaktari kusisitiza kuwa, madaktari  wa Sudan wataendelea na mgomo wa nchi nzima mpaka yatakaposikilizwa matakwa yao.

Madaktari nchini Sudan wanalalamikia kutiwa nguvuni wenzao kwa sababu zisizo za kimsingi

 

Mgomo wa nchi nzima wa madaktari katika vituo vya afya na tiba nchini Sudan ulianza tarehe 6 Oktoba mwaka huu na ulikuwa ukifanywa mara tatu kwa wiki.

Hata hivyo baada ya serikali kulegeza kamba, mgomo wa madaktari hao umesimamishwa kwa muda na madaktari hao watarejea kazini kama kawaida.

Kutiwa mbaroni madaktari ilikuwa ni hatua isiyo sahihi ya vyombo vya dola na ndio maana ilizusha hasira za madaktari kote nchini Sudan.

Ukitoa mgomo wa madaktari, wananchi wa Sudan wanaendelea na malalamiko yao dhidi ya kupandishwa gharama za nishati pamoja na hali ya kisiasa na kijamii nchini mwao.