Upinzani dhidi ya serikali waongezeka nchini Sudan
Upinzani dhidi ya serikali ya Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan unaripotiwa kuongezeka huku polisi na vikosi vya usalama vya nchi hiyo vikitumia mabavu kukabiliana na upinzani huo.
Jumuiya za kiraia nchini Sudan zimetoa taarifa na kutangaza kuwa, katu hazitasalimu amri mbele ya maamuzi mapya ya serikali ya Khartoum bali zitaendelea kushinikiza ili Rais al-Bashir wa nchi hiyo atazame upya suala la kukandamiza harakati za kisiasa na kijamii nchini humo.
Hatua za kukandamiza harakati za kisiasa na kijamii sambamba na kutiwa mbaroni wanaharakati wa kisiasa ambazo zinashuhudiwa hivi sasa nchini Sudan zimetokana na kuongezeka bei za bidhaa na kupungua kiwango cha uwezo wa kununua wa raia. Maandamano ya kupinga hatua za ukandamizaji za serikali ya Sudan yamekuwa yakikabiliwa na mkono wa chuma wa vyombo vya usalama vya nchi hiyo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, hatua hizo za vyombo vya usalama vya Sudan zimepelekea kuibuka anga ya mvutano baina ya wapinzani na vyomba vya dola.
Vuta nikuvute baina ya wapinzani na vikosi vya usalama inaripotiwa siku moja tu baada ya serikali ya Sudan kuwatia mbaroni viongozi wanne mashuhuri wa upinzani nchini humo akiwemo mwanasiasa mkongwe Sadiq Youssef.
Maandamano na upinzani dhidi ya serikali nchini Sudan umeshadidi zaidi baada ya serikali ya Khartoum kufuta ruzuku ya wananchi katika sekta ya nishati, suala ambalo limesababisha kupanda bei ya bidhaa muhimu na hivyo kushuhudiwa ughali mkubwa wa maisha.