UN: Hali ya mambo Jamhuri ya Afrika ya Kati inatia wasiwasi
Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la ukatili na takwimu za mauaji ya raia katika mapigano yaliyoanza wiki iliyopita katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mshauri Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Kuzuia Mauaji ya Kimbari, Adama Dieng, ametoa taarifa akisema kuwa, wanamgambo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu Jumamosi iliyopita wameua raia 85 wa kundi la Peule. Taarifa hiyo imesema kuwa, raia wengine 76 wamejeruhiwa na wengine elfu 11 wamelazimika kukimbia makazi na nyumba zao.
car
Adama Dieng ameeleza wasiwasi wake kuhusu ukatili na mauaji hayo na kutoa wito wa kusitishwa mapigano katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mji wa Bria ulioko kakazini mashariki mwa Bangui tangu Jumamosi iliyopita umekumbwa na mapigano makali baina ya wanachama wa makundi mawili ya wanamgambo wa Seleka. Ripoti zinasema kuwa wahanga wengi wa mapigano hayo ni watu wa kundi la Peule.