Mkutano wa 16 wa Francophone waanza leo nchini Madagascar
Mkutano wa 16 wa wanachama katika Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa (Francophone) umeanza leo Jumamosi katika mji mkuu wa Madagascar, Antananarivo.
Rais Hery Rajaonarimampianina wa Madagascar amesema katika kikao cha ufunguzi wa mkutano huo kwamba, nchi wanachama katika jumuiya ya Francophone zinataka kufanyike juhudi za kuimarisha haki na uadilifu kote duniani.
Rajaonarimampianina ameongeza kuwa, njia na ubunifu wa kisiasa ndiyo inayoweza kudhibiti wimbi kubwa la wahamiaji kutoka nchi za Kiafrika kuelekea Ulaya.
Viongozi wa karibu nchi 30 wanachama katika Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kifaransa (Francophone) wanashiriki katika mkutano wa Antananarivo.
Kabla ya kuanza mkutano huo Katibu Mkuu wa jumuiya ya Francophone, Michaelle Jean alitoa wito wa kutanguliza mbele ubinadamu katika kukabiliana na mgogoro wa wahajiri.
Viongozi wa nchi zinazoshiriki katika mkutano huo wanajadili maudhui za ustawi, maendeleo yanayoambatana na kuwajibika na masharti ya kuwepo amani na utulivu dunia na katika nchi wanachama.