Vyama vya upinzani Sudan vyataka Rais al-Bashir aondoke madarakani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20668-vyama_vya_upinzani_sudan_vyataka_rais_al_bashir_aondoke_madarakani
Vyama vya upinzani nchini Sudan vimetangaza kuwa, Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir hana sifa za kuendelea kuiongoza nchi hiyo hivyo anapaswa kuondoka madarakani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 03, 2016 10:40 UTC
  • Vyama vya upinzani Sudan vyataka Rais al-Bashir aondoke madarakani

Vyama vya upinzani nchini Sudan vimetangaza kuwa, Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir hana sifa za kuendelea kuiongoza nchi hiyo hivyo anapaswa kuondoka madarakani.

Chama cha upinzani cha Harakati Kwa Ajili ya Ukombozi wa Watu wa Sudan ambacho hivi karibuni kimetangaza kuwa pamoja na vyama vingine vya upinzani kimeeleza kuwa, kiko tayari kushirikiana na asasi za kimataifa kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kumuondoa madarakani Rais Omar Hassan al-Bashir wa nchi hiyo.

Hatua hiyo ya vyama vya upinzani ya kuendelea kushinikiza Rais al-Bashir aondoke madarakani inatajwa kuwa changamoto  ya kisiasa dhidi ya Rais wa nchi hiyo. Harakati hizo za vyama vya upinzani zinafanyika katika hali ambayo, katika siku za hivi karibuni miji mbalimbali ya Sudan imeshuhudia kuongezeka upinzani dhidi ya serikali ya Khartoum.

Rais Omar al-Bashir wa Sudan

Maandamano dhidi ya serikali yanazidi kushika kasi nchini Sudan katika hali ambayo, maelfu ya raia wa taifa hilo wanataka kukomeshwa mpango wa kutekelezwa siasa za kubana matumizi sanjari na kufanyika marekebisho ya kiutawala. 

Asasi za kiraia nchini Sudan zinasisitiza kuwa, kamwe wananchi hawatokubaliana na maamuzi mapya ya serikali na badala yake zitaendeleza juhudi zake za kumlazimisha Rais Omar al-Bashir wa nchi hiyo aangalie upya sera za serikali yake.