Mahakama ya Ufaransa yapasisha miaka 25 jela dhidi ya Simbikangwa
-
Pascal Simbikangwa, mahakamani nchini Ufaransa
Mahakama moja nchini Ufaransa imepasisha kifungo cha miaka 25 jela dhidi ya mkuu wa zamani wa usalama wa taifa wa Rwanda baada ya kumpata na hatia ya kufanya mauaji ya kimbari mwaka 1994 nchini humo.
Pascal Simbikangwa (56) ambaye alikuwa askari wa kikosi cha ulinzi wa Rais wa Rwanda amepatikana na hatia pia ya kufanya jinai dhidi ya binadamu kabla ya kukata rufaa mwezi Oktoba. Hivi sasa mahakama ya Ufaransa imerupilia mbali rufaa yake na kupasisha hukumu ya kufungwa jela miaka 25.
Wimbi la mauaji ya kimbari liliikumba Rwanda mwaka 1994 baada ya kutunguliwa ndege ya Juvenal Habyarimana, rais wa wakati huo wa Rwanda karibu na Kigali. Habyarimana alikuwa anarejea nchini humo kutokea Arusha Tanzania alikofikia makubaliano na wapinzani.
Mauaji ya kimbari ya Rwanda yanahesabiwa kuwa ni maafa makubwa zaidi ya kibinadamu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Karibu watu milioni moja hasa wanawake na watoto wadogo waliuliwa kinyama na Wahutu wenye misimamo mikali. Wanawake na watoto karibu 200 hadi 500 walinajisiwa kwenye jinai hiyo ya kutisha.