Kenya yakanusha madai ya kutekwa mji wake mpakani na Somalia
Vyombo vya usalama nchini Kenya vimekadhibisha habari zilizoenea katika mitandao ya kijamii kuwa mji wa Elwak ulioko katika mpaka wa nchi hiyo na Somalia umetekwa na wanamgambo wa kigaidi wa al-Shabaab.
Bernard Nyakwaka, Kamanda Mkuu wa Polisi katika kaunti ya Mandera amesema habari hizo za tetesi kuwa mji wa Elwak uko mikokoni mwa al-Shabaab ni propaganda na uvumi.
Ameliambia gazeti la Nation kuwa binafsi amewasiliana na Dan Chacha, OCPD wa eneo hilo ambaye amemhakikishia kuwa mji huo una utulivu na wala hakuna habari zozote za kutekwa kwake.
Baadhi ya wakaazi wa mji huo wamechapisha katika kurasa zao za mitandao ya kijamii hususan Twitter, wakidai kuwa mji wa Elwak jana ulishuhudia makabiliano makali kati ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na maafisa usalama. Wengine wanadai kuwa taharuki imetanda katika mji huo na kwamba kwa sasa unadhibitiwa na wapigajani wa al-Shabaab, waliotoka nchi jirani ya Somalia.
Wakaazi wengine wa mji wa Elwak wameviambia vyombo vya habari kuwa wanajeshi wa Somalia wamevuka mpaka na kuingia nchini Kenya eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo, ili kuwakabili magaidi hao.
Haya yanaarifiwa siku chache baada ya Mratibu wa serikali ya Kenya katika eneo la Kaskazini Mashariki Mohamud Saleh, kusema kuwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo vinapanga kutekeleza mpango wa kukusanya silaha katika maeneo ya nchi hiyo yanayopakana na nchi za Somalia na Ethiopia, hususan miji ya Mandera, Wajir na Garissa.
Si vibaya kukumbusha hapa kuwa, mwaka 2011, Kenya ilituma wanajeshi wake wa KDF nchini Somalia kushiriki katika oparesheni ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika chini ya mwavuli wa AMISOM, baada ya magaidi wa al-Shabaab kufanya mashambulizi kadhaa ya kigaidi nchini humo sambamba na kuwateka nyara watalii.