Wanaharakati: Rais Buhari anakiuka haki zote za Mashia Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i2203-wanaharakati_rais_buhari_anakiuka_haki_zote_za_mashia_nigeria
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesema serikali ya nchi hiyo imekiuka haki zote za msingi za Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 01, 2016 04:31 UTC
  • Wanaharakati: Rais Buhari anakiuka haki zote za Mashia Nigeria

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesema serikali ya nchi hiyo imekiuka haki zote za msingi za Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo.

Msemaji wa harakati hiyo, Musa Said amesema Rais Muhamadu Buhari wa nchi hiyo amekataa kuheshimu sheria za msingi za nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Kishia. Katika mahojiano na shirika la habari la AFP, Musa amesema kuendelea kuzuiliwa kwa kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na idadi kubwa ya wafuasi wake pasina kufunguliwa mashtaka ni ukiukaji wa wazi wa haki zao za msingi na kukanyagwa kwa sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu. Msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, Sheikh Zakzaky pamoja na makumi ya wafuasi wake wanazuiliwa kwa zaidi ya siku 70 sasa, pasina kufunguliwa mashtaka na kutoruhusiwa kuwa na mawakili. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch katika ripoti yake ya hivi karibuni, lililaani mauaji na ukandamizaji uliofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji wa Zaria mwishoni mwa mwaka jana.

Itakumbukwa kuwa, tarehe 12 hadi 14 Disemba mwaka uliopita wa 2015, jeshi la Nigeria lilishambulia kituo cha kidini na nyumba ya kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky katika mji wa Zaria na kuua mamia ya Waislamu wasio na hatia. Hatima ya Sheikh Zakzaky ambaye alipigwa risasi kadhaa katika hujuma hiyo, bado haijajulikana mpaka sasa.