Polisi ya Nigeria: Tutapambana kwa nguvu zote na magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22507-polisi_ya_nigeria_tutapambana_kwa_nguvu_zote_na_magaidi
Polisi ya Nigeria imesisitiza katika tangazo lake maalumu kwamba, imezimia kwa dhati kupambana kwa nguvu zake zote na magaidi na makundi yanayojihusisha na vitendo vya kuwateka nyara watu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 31, 2016 11:28 UTC
  • Polisi ya Nigeria: Tutapambana kwa nguvu zote na magaidi

Polisi ya Nigeria imesisitiza katika tangazo lake maalumu kwamba, imezimia kwa dhati kupambana kwa nguvu zake zote na magaidi na makundi yanayojihusisha na vitendo vya kuwateka nyara watu.

Msemaji wa Wizara ya Usalama ya Nigeria, Tony Opuiyo ametangaza kuwa, vikosi vya usalama vya nchi hiyo vimeandaa mikakati ya kupambana na magaidi na makundi yanayohatarisha usalama wa nchi hiyo kwa kuwateka nyara watu.

Amesema kuwa, askari usalama wa Nigeria wameanzisha operesheni maalumu dhidi ya ugaidi  na wakiwa na lengo la kudhamini amani na usalama wa raia wamekusudia kupambana na watekaji nyara, magaidi na makundi mengine yanayotenda jinai nchini humo.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Usalama ya Nigeria, kuna kundi moja linalojihusisha na vitendo vya utekaji nyara watu katika barabara kuu baina ya majimbo ya Edo na Kogi kusini mwa nchi hiyo ambalo limehatarisha usalama na amani ya maeneo hayo na kuzusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia.

Tony Opuiyo amesema pia kuwa, vikosi vya usalama vya Nigeria vimewatia mbaroni watu kadhaa wanaodhaniwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake Nigeria mwaka 2009, watu zaidi ya elfu 20 wamepoteza maisha kutokana na hujuma za kundi hilo la magaidi wakufurishaji nchini Nigeria. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram.