Amnesty yaitaka Sudan iache kukiuka haki za wanafunzi wa Vyuo Vikuu
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limeitaka serikali ya Sudan ikomeshe dhulma na ukandamizaji dhidi ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini humo na hususan katika jimbo la Darfur.
Shirika la habari la Tasnim limeandika kuhusu ripoti iliyotolewa na Amnesty International jana Jumatano ambayo imesema kuwa, tangu mwaka 2003, zaidi ya wanchuo 10,000 wamekamatwa na kuzuiliwa kinyume cha sheria huku wengine 13 wakiuawa, katika kile kinachotajwa kuwa hujuma za kisiasa.
Muthoni Wanyeki, Mkurugenzi wa Amnesty International kanda ya Afrika Mashariki amesema: "Hujuma hizi za makusudi na za fedheha dhidi ya wanachuo ni jambo lisilokubalika na ambalo lazima likomeshwe haraka iwezekanavyo."
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, watu zaidi ya laki tatu wameuawa katika machafuko ya Darfur yaliyoanza mwaka 2003 na wengine milioni mbili na nusu wamelazimika kuwa wakimbizi.
Aidha mashirika mbalimbali ya utoaji misaada ya kibinadamu yamekuwa yakitahadharisha mara kwa mara kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu katika jimbo hilo na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kuzuia kutokea maafa ya kibinadamu.
Ripoti ya Amnesty International iliyotolewa Septemba mwaka jana ilieleza kuwa, vikosi vya serikali ya Sudan vilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia baina ya mwezi Januari hadi Septemba mwaka 2016 katika mashambulio yake dhidi ya waasi huko Darfur.