UN: Watu milioni 5.6 wanakabiliwa na njaa Ethiopia
Umoja wa Mataifa umesema mamilioni ya watu wako katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na athari za kiangazi na ukame nchini Ethiopia.
Stephen O'Brien, Mkuu wa Ofisi ya Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa amesema ukame huo umesababisha Waethiopia milioni 5.6 wahitajie misaada ya dharura.
Afisa huyo wa UN ametahadharisha kuwa, iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa, idadi kubwa ya watu watapoteza maisha kutokana na njaa kama ilivyoshuhudiwa mwaka jana.

Kiangazi cha mwaka jana kilisababisha watu milioni 10.2 kukabiliwa na njaa, utapiamlo na lishe duni, huku mamia ya maelfu ya wengine wakifariki dunia kutokana na njaa nchini Ethiopia.
Mitiku Kassa, Mkuu wa Kitengo cha Kukabiliana na Majanga nchini Ethiopia amesema nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inahitajia msaada wa dola milioni 948 za Marekani kutoka jamii ya kimataifa, ili kudhibiti ukame na baa la njaa.
Ripoti ya hivi karibuni ya shirika la Save the Children ilisema kuwa, upungufu wa mvua za kutosha ulioshuhudiwa kwa miaka kadhaa mtawalia, umesababisha zaidi ya watu milioni 15 katika nchi za Somalia, Ethiopia na Kenya kukumbwa na mgogoro wa chakula, aghalabu yao wakiwa ni watoto.