12 wauawa katika mapigano Jamhuri ya Afrika ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i2551-12_wauawa_katika_mapigano_jamhuri_ya_afrika_ya_kati
Watu 12 wameuliwa na watu wenye silaha katika vijiji vya Jamhuri ya Afrika ya Kati, katika mapigano ya kwanza tangu Faustin-Archange Touadera kuidhinishwa kuwa rais wa nchi hiyo, Jumanne iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 06, 2016 12:59 UTC
  • 12 wauawa katika mapigano Jamhuri ya Afrika ya Kati

Watu 12 wameuliwa na watu wenye silaha katika vijiji vya Jamhuri ya Afrika ya Kati, katika mapigano ya kwanza tangu Faustin-Archange Touadera kuidhinishwa kuwa rais wa nchi hiyo, Jumanne iliyopita.

Habari zinasema kuwa, mauaji hayo ya usiku wa kuamkia leo yametokea katika vijiji vilivyoko mjini Bambari, katikati mwa nchi hiyo. Imearifiwa kuwa, watu 6 wameuawa katika vijiji vitatu tofauti vya mji huo, katika kile kinachoaminika kuwa ni mapigano ima ya wizi wa mifugo au vita vya kikabila.

Habari zaidi zinasema kuwa, wanawake watatu wa familia moja wameuawa kwa kuchinjwa katika eneo lililoko yapata kilomita 6 kutoka mji wa Bambari. Mauaji haya mapya yametokea siku chache baada ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Katikati mwa Afrika na vile vile Umoja wa Nchi Zinazozungumza Kifaransa (Francofone) kutoa taarifa ya pamoja zikiunga mkono kuidhinishwa matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati iliudhinisha ushindi wa Rais mpya wa nchi hiyo, Faustine Archange Touadera katika uchaguzi wa rais wa Februari 14 mwaka huu na kupinga ombi la aina yoyote la vyama vya upinzani la kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo.

Katika kampeni zake, Rais mteule Faustin Touadera aliahidi kuimarisha usalama na kuzima vita vya kikabila na kidini ambavyo vimeikumba nchi hiyo ya katikati mwa Afrika kwa muda mrefu sasa.