Muda wa usitishwaji vita waongezwa Msumbiji
Chama kikuu cha upinzani Msumbiji, Renamo, ambacho pia ni harakati ya waasi, kimeongeza muda wa usitishwaji mapigano kwa miezi mingine miwili ili kutoa mwanya wa mazungumzo na serikali ya Rais Filipe Nyusi.
Taarifa hiyo ya Renamo iliyotolewa Ijumaa imeongeza matumaini ya kupatikana amani katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika ambayo imekuwa ikishuhudia mapigano ya mara kwa mara ya waasi hao na vikosi vya serikali.
Msumbiji imekuwa ikitawaliwa na chama cha Frelimo tangu ilipopata uhuru na kiongozi wa waasi wa zamani wa Renamo Afonso Dhlakama amekuwa akishindwa katika uchaguzi wa rais tangu mwaka 1994 na chama hicho kubakia kuwa ni harakati kuu ya upinzani.
Vyama vya Renamo na Frelimo vilipigana vita vya ndani kutoka mwaka 1976 hadi 1992 ambapo watu milioni moja walipoteza maisha kabla ya kutiwa saini mapatano ya amani.
Renamo iliendelea kuwa na kundi la wanamgambo ambao wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya hapo na pale tokea mwaka 2014 wakati Renampo ilikataa kukubali matokeo ya uchaguzi. Kiongozi wa Renamo, Afonso Dhlakama akizungumza na waandishi habari akiwa mafichoni kati mwa Msumbuji amesema muda wa usitishwaji vita utaendelea hadi Mei 4 kutoka Januari 2.
Rais Nyusi anatazamia pande mbili zitakuwa na mapatano ya muda mrefu ili kuimarisha nafasi yake wakati wa mkutano wa kilele wa chama tawala cha Frelimo Mwezi Septemba ambao wanatazamiwa kuteuliwa kugombea urais.