Tanzania kupeleka madaktari 500 Kenya kusaidia kukabiliana na mgomo
Tanzania itapeleka madaktari 500 Kenya kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na athari za mgomo wa madaktari unaoendelea katika hospitali za umma.
Hayo yameelezwa leo katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais na kufafanua kwamba: "Tanzania imekubali ombi la Kenya la kupatiwa madaktari 500 kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na uhaba wa madaktari katika vituo vyake vya tiba kufuatia mgomo wa madaktari".
Taarifa hiyo imeongeza kuwa serikali ya Kenya itawalipa madaktari hao wa Tanzania na kuwapatia makaazi. Kwa mujibu wa Waziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu nchi hiyo ina madaktari wengi wenye sifa zinazostahili lakini hawana ajira.
Rais John Magufuli ameidhinisha utekelezaji wa ombi la serikali ya Kenya la kupatiwa madaktari baada ya kukutana na Waziri wa Afya wa nchi hiyo Cleopas Mailu mjini Dar es Salaam leo.
"Matatizo ya Kenya ni matatizo ya Tanzania", ameeleza rais Magufuli.
Madaktari wa Kenya katika hospitali za umma walianzisha mgomo tarehe 5 Desemba mwaka uliopita kulalamikia mishahara na mazingira ya kazi. Hii ni katika hali ambayo makubaliano yaliyosainiwa wiki hii yamefungua njia kwa mazungumzo ya kuhitimisha mgomo huo, hata hivyo madaktari wengine bado hawajarudi makazini.
Mgomo huo umesababisha hospitali nyingi za umma ambazo tayari zina matatizo ya fedha na vifaa kutowapokea baadhi ya wagonjwa. Muuguzi mmoja alivieleza vyombo vya habari hapo jana kuwa kulikuwepo na madaktari wawili tu wakati huo katika hospitali ya taifa ya Kenyatta jijini Nairobi ambayo ndiyo hospitali kubwa zaidi ya umma nchini humo.
Hali hiyo imetishia kudhoofisha juhudi za Rais Uhuru Kenyatta za kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu…/