Rais wa Ghana atetea uamuzi wake wa kuteua mawaziri 110
Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo amewakosoa vikali wapinzani wake na wanaharakati wanaopinga hatua yake ya kuwateua mawaziri zaidi ya 100 katika serikali yake mpya.
Rais wa Ghana amesema uamuzi wake wa kuwateua mawaziri 110 ni mkakati wa dharura na mpango unaonuia kuinua uchumi wa nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika.
Rais Nana Akufo-Addo ambaye alishinda uchaguzi wa rais Disemba mwaka jana amesema: "Niliahidi kunyanyua kiwango cha uchumi wa nchi na kupambana na ufisadi. Hawa mawaziri niliowateua wanakuja kuchapa kazi, hawaji likizo."
Wapinzani na wakosoaji wa serikali nchini humo hususan katika mitandao ya kijamii wamemshutumu Rais Akufo-Addo kwa hatua yake hiyo ya kuteua baraza kubwa la mawaziri licha ya nchi hiyo kukabiliwa na misukosuko ya uchumi.
George Lawson, Naibu Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha National Democratic Congress (NDC) amelaani vikali uamuzi huo wa Akufo-Addo, na kusema kuwa, huko ni kuusambaratisha zaidi uchumi wa nchi kwa maslahi ya 'kuwalipa' wapambe wake waliomsaidia katika kampeni za urais.
Katika uchaguzi huo wa Disemba mwaka jana, Akufo-Addo alipata asilimia 53.8 ya kura na kumbwaga Rais wa wakati huo John Dramani Mahama, aliyezoa asilimia 44.4 ya kura zote.