Tunisia yaangamizi Madaesh wengine 5 karibu na mpaka na Libya
Jeshi la Tunisia limesema kuwa limefanikiwa kuangamiza wanamgambo wengine watano wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh karibu na mpaka wa nchi hiyo na Libya.
Taarifa iliyotolewa jana jioni na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imesema kuwa, maafisa wa usalama wamewaangamiza magaidi watano wa Daesh katika operesheni kali iliyofanyika katika eneo la Benniri, mashariki mwa mji wa Ben Guerdane. Operesheni hiyo imefanyika saa chache baada ya jeshi la nchi hiyo kukamata watu 17, wanaotuhumiwa kuwa magaidi wa Daesh, karibu na kambi ya jeshi iliyoko katika eneo hilo. Waziri Mkuu wa Tunisia Habib Essid amethibitisha habari hizo na kusema kuwa, askari 12 waliuawa katika hujuma ya Daesh dhidi ya kambi ya jeshi katika eneo la Ben Guerdane siku ya Jumatatu. Watu zaidi ya 50 waliripotiwa kuuawa katika mapigano hayo kati ya vikosi vya jeshi la Tunisia na magaidi wa Daesh. Kufuatia mapigano hayo, maafisa wa serikali ya Tunis walitangaza marufuku ya kutoka nje na kuwataka wakaazi wa mji huo wa Ben Guerdan wabaki majumbani mwao. Mara kwa Mara Tunisia imekuwa ikikabiliwa na tishio la makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao katika nchi jirani ya Libya. Raia kadhaa wa Tunisia wamejiunga na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh; na magenge kadhaa yenye mfungamano na kundi hilo yameshatiwa mbaroni.