Mabaharia kadhaa wa India watekwa nyara katika fukwe za Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27236-mabaharia_kadhaa_wa_india_watekwa_nyara_katika_fukwe_za_somalia
Afisa mmoja anayehusika na vita dhidi ya maharamia wa baharini nchini Somalia ametangaza habari ya kutekwa nyara mabaharia 11 wa India katika fukwe za Somalia.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 03, 2017 09:52 UTC
  • Mabaharia kadhaa wa India watekwa nyara katika fukwe za Somalia

Afisa mmoja anayehusika na vita dhidi ya maharamia wa baharini nchini Somalia ametangaza habari ya kutekwa nyara mabaharia 11 wa India katika fukwe za Somalia.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Graeme Gibbon-Brooks, afisa wa shirika la kujitegemea la Dryad Maritime Security la kupambana na maharamia nchini Somalia akisema leo kuwa, meli ya biashara ya India iliyokuwa na mabaharia 11 raia wa nchi hiyo ambayo ilikuwa inatokea Dubai kuelekea Boosaaso, kaskazini mwa Somalia imevamiwa na kutekwa nyara na maharamia katika fukwe za Somalia.

Graeme ameongeza kuwa, meli hiyo ya biashara ya India imepelekwa kwenye eneo la Eyl la kaskazini mwa Somalia.

Kutekwa nyara meli za mafuta na biashara ni mgogoro mkubwa nchini Somalia.

 

Afisa huyo wa shirika binafsi la kupambana na maharamia nchini Somalia ameongeza kuwa, maharamia hao wametaka walipwe fedha za kukombolewa mabaharia hao wa India.

Hili ni tukio la karibuni kabisa la kutekwa nyara meli ya biashara na maharamia wa Kisomali ikiwa ni ishara ya kuanza wimbi jipya la kutekwa nyara meli zinazotumia bahari ya Somalia.

Maji ya Somalia katika Bahari ya Hindi ndilo eneo hatari zaidi kwa vyombo vya baharini ulimwenguni.

Magenge ya maharamia yamepata fedha nyingi za vikomboleo kutokana na kuteka nyara meli na mabaharia wa nchi za kigeni katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.