Wafanya magendo ya binadamu watiwa mbaroni Sudan
Kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Sudan ametangaza habari ya kutiwa nguvuni watu watano wanaojihusisha na magendo ya binadamu karibu na mpaka wa nchi hiyo na Libya.
Muhammad Hamdan Kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Sudan amesema kuwa magari sita yaliyokuwa yakitumiwa na watu hao kusafirishia wahamiaji haramu kutoka maeneo ya mipakani yamekamatwa katika oparesheni ya jeshi. Kuhusiana na suala hilo Joel Milman Msemaji wa Shirika la Kimataifa la Wahajiri hivi karibuni alitangaza kuwa mapigano kati ya makundi hasimu yanayoendesha magendo ya binadamu katika pwani ya Libya yamesababisha vifo vya wahajiri 22.
Libya hivi sasa imekuwa kituo cha awali cha kuanzia safari za wahajiri wanaoelekea Ulaya kufuatia Umoja wa Ulaya kuweka vizuizi vikali katika kukabiliana na wimbi la wakimbizi kwa kuwafungia wahajiri mipaka ya Ugiriki katika msimu wa mapukutiko uliopita. Tangu kuanza mwaka huu wa 2017, wanawake, wanaume na watoto wasiopungua laki moja wametumia njia ya bahari ili kuingia Italia wakitokea kaskazini mwa Afrika; hata hivyo watu zaidi ya 3100 walizama baharini wakiwa njiani. Aidha katika kipindi hicho, wafanya magendo ya binadamu chini ya 100 walitiwa mbaroni katika maji ya kimataifa.