Apr 15, 2017 13:44 UTC
  • Makumi ya Waislamu wajeruhiwa  baada ya msikiti kuchomwa moto Algeria

Makumi ya Waislamu nchini Algeria wamejeruhiwa kwa moto, baada ya msikiti waliokuwa wakishwali ndani yake kuchomwa moto makusudi.

Habari kutoka Algeria zinaarifu kwamba, mtu mmoja raia wa nchi hiyo aliuchoma moto msikiti wa mkoa wa Tébessa, wakati Waislamu walipokuwa wakiswali sala ya Ijumaa hapo jana ambapo katika tukio hilo makumi ya Waislamu walijeruhiwa. Kwa mujibu wa habari hiyo, majeruhi hao wamelazwa katika hospitali mkoani hapo wakiendelea na matibabu.

Wakati wa kujiri tukio hilo

Polisi ya Algeria imetangaza kumtia mbaroni mtu huyo mwenye umri wa miaka 35. Hata hivyo polisi hiyo haikufafanua kama mtu huyo ni mwanachama wa makundi ya kigaidi au la. Tukio hilo linajiri zikiwa zimepita siku chache ambapo watu wasiopungua 22 walifariki dunia na wengine zaidi ya 80 kujeruhiwa katika ajali ya moto iliyotokea kwenye Ijitimai ya Waislamu wa Kisufi wa tariqa ya Tijaniyyah huko nchini Senegal.

Waislamu wa Algeria

Moto huo ulitokea kwenye kijiji cha  Médina Gounass katika mji wa Tambacounda kusini mashariki mwa Senegal tarehe 12 mwezi huu sehemu ambayo kila mwaka hufanyika Ijitimai ya maelfu ya Waislamu wa Kisufi wafuasi wa tariqa ya Tijaniyyah kutoka Senegal, Guinea na nchi zingine za Afrika Magharibi. Rais Macky Sall wa Senegal alituma salamu za rambirambi na mkono wa pole kwa familia na watu waliofariki kwenye ajali hiyo.

 

 

 

 

 

 

 

Tags