Uganda yaanza kuondoa vikosi vyake Jamhuri ya Afrika ya Kati
Jeshi la Ulinzi la Uganda UPDF limeanza kuondoa askari wake huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambao wamekuweko nchini humo tangu mwaka 2012.
Kikosi cha kwanza cha UPDF kimepokea leo katika eneo la Gulu na Brigedia Katsigazi Tumusiime, Mkuu wa Vikosi vya Nchi Kavu na Brigedia Emmanuel Kanyesigye, Kamanda Mwandamizi wa Batalioni ya 4 ya jeshi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya UPDF, uamuzi huo wa Uganda kuanza kuondoa vikosi vyake Jamhuri ya Afrika ya Kati umetokona na ukweli kwamba, jeshi la Uganda limefanikiwa pakubwa kuzima harakati za kundi la waasi la LRA kiasi kwamba, haliwezi kuanzisha vita vyovyote dhidi ya Uganda.
Msemaji wa Jeshi la Uganda, Brigedia Richard Karemire amesema mustakabali na utulivu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa sasa ipo mikononi mwa serikali na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.
Novemba mwaka jana, Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa ilitangaza kumalizika rasmi muda wa kuhudumu wanajeshi wa nchi hiyo huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Baada ya tangazo hilo, shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) liliutaka Umoja wa Mataifa kuimarisha ulinzi wa raia katika nchi hiyo na kusisitiza kuwa, umoja huo unapaswa kuimarisha kikosi cha askari wake walioko katika nchi hiyo chini ya mwavuli wa MINUSCA.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika mgogoro mwaka 2013 baada ya kuzuka mapigano ya kikaumu yaliyopelekea kuondolewa madarakani serikali ya Rais François Bozizé.