Uislamu unaenea kwa kasi nchini Zimbabwe
Uislamu unaenea kwa kasi nchini Zimbabwe huku wakaazi wengi wa nchi hiyo wakiwa sasa wanafahamu na kukubali mafundisho ya dini hiyo tukufu.
Katika mahojiano na gazeti la Sunday Mail la Zimbabwe, Sheikh Shaibu Asali, Mkuu wa Kitengo cha Kiarabu cha Chuo cha Kiislamu Harare amesema, kati ya wakaazi wote milioni 15 wa nchi hiyo, karibu asilimia tatu ni Waislamu.
Ameongeza kuwa ingawa Waislamu bado ni wachache lakini hivi sasa wameanza kuongezeka katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya Wakristo na watu wa dini za jadi.
Amesema katika miaka ya huko nyuma ni watu wachache waliokuwa wakiufahamu Uislamu kwani kulikuwa na sera za kuwapinga Waislamu hasa vijijini. Hata hivyo hali hiyo imebadilika kwani kuna vitabu vingi kuhusu Uislamu ambavyo vimesambazwa kote Zimbabwe. Aidha amesema katiba ya mwaka 2013 ya Zimbabwe inaruhusu uhuru wa kuabudu na hivyo kuondoa ile dhana iliyokuwepo miaka ya nyuma kuwa Uislamu ni dini ya wageni. Sheikh Asali anasema kuna misikiti 20 Harare, misikiti minane Bulawayo na mingine mingi kote Zimbabwe.