May 16, 2017 14:22 UTC
  • Walioambukizwa Ebola waongezeka DRC, wafika 20

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC idadi ya visa vinavyoshukiwa kuwa ni Ebola imeongezeka na kufikia 20.

Shirika la Afya Dunini WHO limesema kati ya visa hivyo shukiwa, visa viwili vimethibitishwa katika maabara ya taifa kuwa ni Ebola na idadi ya waliofariki dunia imesalia kuwa ni watu watatu.

Msemaji wa WHO mjini Geneva, Uswisi, Christian Lindmeier amesema jopo la wataalamu wa afya kutoka wizara ya afya nchini DRC linaendelea na uchunguzi huko Likati kwenye jimbo la Bas-Ulele kwa ushirikiano na wataalamu wa shirika hilo. Ameongeza kuwa hivi sasa kuna watu 400 wanaofuatiliwa kwa uchunguzi kwenye maeneo manne tofauti, na sampuli mpya tano zimekusanywa na kwamba zitafanyiwa uchunguzi hivi punde.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Daktari Matshidiso Moeti ameutembelea mji mkuu wa DRC, Kinshasa na kusema timu ya wataalamu wa afya watatumwa katika eneo ambalo Ebola imeibuka mpya katika mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Maziko ya mtu aliyepoteza maisha baada ya kuugua Ebola

Mnamo mwaka 2014, mkurupuko wa ugonjwa huo Congo DR ulidhibitiwa kwa haraka ingawa watu 49 walifariki dunia. Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 11,000 walifariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa  wa Ebola katika eneo la Afrika Magharibi mwaka 2014 hadi 2015, hususan nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia katika mlipuko wa Ebola ulioatajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani. Ebola ni aina ya ugonjwa ambao mgonjwa hutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili na ambao huambukizwa mtu iwapo atagusana moja kwa moja na damu au maji maji yanayotoka mwillini mwa mgonjwa.

 

Tags