Ripoti: Watoto wakimbizi wa Sudan wanakabiliwa na lishe duni nchini Chad
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29264-ripoti_watoto_wakimbizi_wa_sudan_wanakabiliwa_na_lishe_duni_nchini_chad
Mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu nchini Chad yametangaza kuwa, watoto wakimbizi wa Sudan walioko katika kambi za wakimbizi nchini humo wanakabiliwa na hali mbaya ya lishe duni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 18, 2017 22:56 UTC
  • Ripoti: Watoto wakimbizi wa Sudan wanakabiliwa na lishe duni nchini Chad

Mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu nchini Chad yametangaza kuwa, watoto wakimbizi wa Sudan walioko katika kambi za wakimbizi nchini humo wanakabiliwa na hali mbaya ya lishe duni.

Wafanyakazi wa mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu wamesema kuwa, hali hiyo ya lishe duni inayowakabili watoto wakimbizi wa Kisudan inatokana na kupungua milo ya chakula kwa watoto hao katika miaka ya hivi karibuni.

Aidha ripoti zinasema kuwa, hali ya wakimbizi katika kambi ya wakimbizi ya Ouré Cassoni iliyoko katika mpaka wa Sudan na Chad ni mbaya na kwamba, wanahitajia misaada ya haraka ya kibinadamu.

Wakimbizi hao ambao ni raia wa Sudan wamekuweko katika kambi hiyo ya wakimbizi tangu mwaka 2003 wakati yalipozuka machafuko katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur. 

Wakimbizi nchini Chad

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, watu zaidi ya laki tatu wameuawa katika machafuko ya Darfur yaliyoanza mwaka 2003 na wengine milioni mbili na nusu wamelazimika kuwa wakimbizi.

Mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu yamekuwa yakitahadharisha mara kwa mara kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu katika eneo hilo.

Wakimbizi wa Darfur walioko huko Chad ni changamoto nyingine kwa nchi hiyo ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa amani kutokana na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram na wakati huo huo wimbi la wakimbizi wanaoingia nchini humo wakitokea Jamhuri ya Afrika ya Kati na Niger.