Sisitizo la Ufaransa la kuendelea kuwepo nchini Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29368-sisitizo_la_ufaransa_la_kuendelea_kuwepo_nchini_mali
Katika safari yake ya kwanza barani Afrika, rais mpya wa Ufaransa Emmanuel Macron amesisitizia juu ya kuendelea kuwepo askari wa nchi yake nchini Mali kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 21, 2017 02:47 UTC
  • Sisitizo la Ufaransa la kuendelea kuwepo nchini Mali

Katika safari yake ya kwanza barani Afrika, rais mpya wa Ufaransa Emmanuel Macron amesisitizia juu ya kuendelea kuwepo askari wa nchi yake nchini Mali kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Emmanuel Macron aliyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari akiwa na mweyeji wake Rais Ibrahim Boubacar Keïta wa Mali ambapo ameelezea juu ya kuendelezwa ushirikiano wa kidiplomasia na kisiasa wa nchi mbili hizo. Aidha amesema kuwa, Paris inaunga mkono suala zima la kuimarishwa usalama na amani nchini Mali na nchi zote za eneo la pwani ya Magharibi mwa Afrika. Kadhalika rais huyo mpya wa Ufaransa ametoa ahadi ya msaada wa Euro milioni 470 kwa ajili ya kustawisha eneo hilo kando na harakati za kijeshi.

Emmanuel Macron akizungumza na askari wa nchi yake walioko Mali

Matamshi ya Emmanuel Macron yanatolewa katika hali ambayo tangu mwanzo nchi yake imekuwa ikishirikiana na serikali ya Bamako katika kile kinachotajwa kuwa ni kupambana na ugaidi nchini Mali. Aidha uingiliaji huo wa kijeshi wa Ufaransa na uepo wa askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa, hadi sasa haujasaidia lolote katika kutatua mgogoro wa nchi hiyo ya magharibiu mwa Afrika. Tangu mwaka 2012 Mali imekuwa ikikabiliwa na matatizo yaliyotokana na mapinduzi ya kijeshi ambapo baada ya hapo hatua ya makundi ya wabeba silaha na yanayopigania kujitenga kudhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, kumeongeza machafuko hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi. Hata kama utiaji saini wa makubaliano ya amani hapo tarehe 15 Mei mwaka 2015 chini ya upatanishi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, kati ya wawakilishi wa serikali ya Bamako na makundi ya wabeba silaha, ulitazamiwa kurejesha usalama na amani nchini humo, lakini kivitendo makubaliano hayo hayajakuwa na mafanikio ambapo mgogoro huo ungali unaendelea kushuhudiwa katika maeneo ya kaskazini mwa nchi. Akthari ya nchi za Kiafrika zingali zinahesabiwa kuwa ni makoloni ya Ufaransa ambapo licha ya kumalizika rasmi kipindi cha ukoloni ndani ya mataifa mengi ya bara hilo, lakini bado Ufaransa inaendeleza uingiliaji wake katika masuala ya ndani ya nchi hizo kupitia ukoloni mamboleo. Migogoro ya kisiasa, machafuko, vita na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ni sababu kuu ya Ufaransa kuhalalisha uwepo wake kijeshi katika nchi za bara hilo.

Wanamgambo wanaofungua njia ya uingiliaji wa Wamagharibi

 

Katika hali hiyo tangu kulipotokea mgogoro wa kisiasa nchini Mali na kuanza harakati za makundi yanayotaka kujitenga, askari wa Ufaransa kwa namna isiyo rasmi wamepiga kambi nchini humo kwa kisingizio cha kudumisha usalama na amani. Hii ni katika hali ambayo askari wa Ufaransa katika kipindi hiki chote si tu kwamba hawajaweza kuwa na nafasi athirifu katika utatuzi wa mgogoro wa taifa hilo bali baadhi ya weledi wa mambo wamethibitisha kuwepo misaada inayotolewa nyuma ya pazia na nchi hiyo kwa makundi ya hayo hayo yanayopigania kujitenga na magenge mengine ya kigaidi.

Macron akiwa na maelfu ya askari wake Mali

Kwa kisingizio cha kurejesha amani na kupambana na makundi ya kigaidi katika nchi za Kiafrika baadhi ya serikali za Magharibi hususan Ufaransa zinakusudia kuongeza uepo wao katika maeneo yenye mapigano barani humo ili ziweze kufikia malengo yao ya kikoloni ukiwemo uporaji wa vyanzo vya utajiri wa mataifa hayo. Itafahamika kuwa, hivi sasa Ufaransa inakusudia kuwa  nchi yenye nguvu kubwa duniani na ni kwa ajili hiyo ndio maana ikaendeleza satwa yake katika makoloni yake ya zamani kupitia nara ya utoaji misaada ya kibinadamu na eti kuzisaidia nchi hizo kulinda usalama wao. Matamshi ya rais mpya wa Ufaransa Emmanuel Macron juu ya kuendelea kuwepo kijeshi kwa nchi yake huko Mali na ahadi za misaada ya mamilioni ya Euro kwa nchi hiyo, pia yametolewa katika fremu hiyo hiyo ya kuendeleza ukoloni wake mamboleo, kupenda kujitanua na kustawisha nafasi yake ya ushindani barani Afrika.