ICC: Mauaji ya kutisha CAR lazima yakomeshwe
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC amelaani vikali mauaji ya kutisha yanayofanyika Jamhuri ya Afrika ya Kati huku ikitaka mapigano mapya yanayoendelea katika mji wa Bangassou, karibu na mpaka wa nchi hiyo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yasitishwe mara moja.
Fatou Bensouda amesema mapigano kati ya magenge ya waasi wanaobeba silaha yameshtadi nchini humo katika miezi ya hivi karibuni, jambo ambalo linaitiwa wasiwasi mkubwa jamii ya kimataifa.
Amesema jinai za kutisha zinazoshuhudiwa nchini humo zinafuatiliwa kwa karibu na mahakama hiyo na kwamba zinafaa kukomeshwa haraka iwezekanavyo.
Kauli ya Bensouda inajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kulaani kitendo cha vyombo vya habari duniani cha kufumbia macho na kutoakisi kwa uzito habari za mashambulizi na mauaji dhidi ya Waislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu hivi karibuni waligundua miili 115 katika mji wa Bangassou, huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, siku chache baada ya genge la waasi wa Kikristo la Anti-Balaka kuvamia mji huo.
Stephane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, Dkt. Yousef Al-Othaimeen katika nyakati tofauti walilaani vikali mauaji hayo ya kikatili ya Waislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo yalitekelezwa na magaidi wa kundi la Kikristo la Anti-Balaka.