Watu 28 wauawa katika shambulizi dhidi ya basi lililobeba Wakristo Misri
Kwa akali watu 28 wameuawa katika shambulizi linaloaminika kuwa la kigaidi lililolenga basi ambalo lililikuwa limewabeba Wakrsito wa Kikhufti kusini mwa mji mkuu wa Misri, Cairo.
Gavana wa mkoa wa Minya, Essam el-Bedawi ameviambia vyombo vya habari kuwa, watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha za otomatiki wamelimiminia risasi basi hilo lililokuwa likielekea katika Kanisa la Saint Samuel katika mkoa huo, ambapo watu 28 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Naye Khaled Megahed, Msemaji wa Wizara ya Afya wa Misri amethibitisha kutokea shambulizi hilo na kubainisha kuwa, watu 25 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo, baadhi yao wakiwa mahututi kutokana na majeraha mabaya ya risasi.
Hadi tunaenda mitamboni, hakuna kundi lilikuwa limetangaza kuhusika na shambulizi la leo, ingawa genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) limekuwa likifanya hujuma za aina hiyo, dhidi ya Wakristo hususan wa Kikhufti, wanaounda asilimia 10 ya watu milioni 92 wa Misri.
Mwezi uliopita wa Aprili, miripuko ya kigaidi katika makanisa mawili ya mji wa Tanta katikati ya mkoa wa al-Gharbiyah na mjini Alexandria nchini humo yalisababisha watu karibu 50 kuuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa.
Mashambulizi mengi ya kigaidi ya miaka ya hivi karibuni nchini Misri yamekuwa yakifanywa na kundi la Ansar Bait al-Muqaddas lililotangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi la Daesh, na kisha kubadilisha jina na kujiita Wilaya ya Sinai.