Algeria yaitaka Misri isimamishe mashambulio ya anga ndani ya ardhi ya Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29802-algeria_yaitaka_misri_isimamishe_mashambulio_ya_anga_ndani_ya_ardhi_ya_libya
Algeria imeitaka Misri isimamishe mashambulio ya anga inayofanya katika eneo la kaskazini mashariki mwa Libya ikisisitiza kuwa hatua hiyo haitotatua mgogoro wa kiusalama unaoikabili Misri.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 30, 2017 11:01 UTC
  • Algeria yaitaka Misri isimamishe mashambulio ya anga ndani ya ardhi ya Libya

Algeria imeitaka Misri isimamishe mashambulio ya anga inayofanya katika eneo la kaskazini mashariki mwa Libya ikisisitiza kuwa hatua hiyo haitotatua mgogoro wa kiusalama unaoikabili Misri.

Gazeti la Ashruuq linalochapishwa nchini Algeria limezinukuu duru za kidiplomasia na kuandika kuwa shambulio la karibuni lililofanywa na Misri ndani ya ardhi ya Libya limekabiliwa na jibu na radiamali ya Algeria ambapo Rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika amemtaka Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri asimamishe mashambulio ya kijeshi dhidi ya Libya.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya Fayez al-Sarraj amewasiliana moja kwa moja na  Ahmed Ouyahia, mkuu wa ofisi ya Rais wa Algeria akitaka Rais wa nchi hiyo afanye upatanishi kwa ajili ya kusimamisha mashambulio ya Misri dhidi ya eneo la kaskazini mashariki mwa Libya.

Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ( kushoto) na Jeneral Khalifa Haftar, mkuu wa jeshi la taifa la Libya

Wakati huohuo, kituo cha habari cha Middle East Online kimeripoti kuwa viongozi wa Misri walikuwa wameshapanga shambulio dhidi ya eneo la kaskazini mashariki mwa Libya hata kabla ya kushambuliwa basi lililobeba raia wakristo wa Misri na kwamba wameitumia hujuma dhidi ya basi hilo kama kisingizio cha kuhalalisha operesheni ya shambulio la anga dhidi ya Libya.

Siku ya Ijumaa na Jumamosi iliyopita ndege za kivita za jeshi la anga la Misri zilishambulia ngome za wanamgambo katika eneo la Derna kaskazini mashariki mwa Libya.

Siku ya Jumapili, Algeria ilitoa wito wa kufanyika kikao cha pande tatu nchini humo baina ya nchi hiyo, Misri na Tunisia kwa ajili ya kujadili mgogoro wa Libya.../