AU, UN zataka kupunguzwa askari wa kulinda amani Darfur, Sudan
Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa zimependekeza kupunguzwa idadi ya askari wanaohudumu kwenye Kikosi cha pamoja cha AU na UN huko Darfur, nchini Sudan UNAMID.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki ijayo linatazamiwa kujadili mapendekezo ya pamoja yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres na Mkuu wa Kamisheni ya AU, Moussa Faki Mahamat ya kutaka kupunguzwa idadi ya askari jeshi wa UNAMID kwa asilimia 44 na idadi ya polisi wa kikosi hicho kwa asilimia 33.
Hii ni katika hali ambayo, Februari mwaka huu, Aristide Nononsi, mtaalamu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Sudan baada ya kufanya safari nchini humo alisema eneo la Darfur ambalo kwa miaka mingi limekumbwa na mauaji na machafuko na kisha kushuhudia usalama wa muda mfupi, limeanza kukabiliwa na machafuko na mauaji ya kikabila.
Askari 64 wamepoteza maisha wakihudumu chini ya mwavuli wa UNAMID tangu kikosi hicho kipelekwe Darfur mwaka 2007, kwa lengo la kulinda raia na kurudisha utulivu katika eneo hilo.
Umoja wa Mataifa unakisia kuwa zaidi ya watu laki tatu wamepoteza maisha na wengine milioni mbili na laki 6 wakilazimika kuwa wakimbizi kutokana na machafuko ya karibu miaka 13 sasa katika jimbo hilo.
UNAMID ina askari 20,000 kutoka nchi 30 duniani ambapo kikosi hicho mwaka jana kiliongozewa muda mwingine wa mwaka mmoja wa kuhudumu nchini Sudan hadi mwisho wa mwezi huu wa Juni wa 2017.