Algeria kuimarisha ushirikiano na Iran katika vita dhidi ya ugaidi
Algeria imelaani vikali mashambulizi pacha ya kigaidi yaliyotokea hivi karibuni hapa mjini Tehran na kusema kuwa, itaendelea kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vita vya kuyatokomeza magenge ya kigaidi.
Hayo yamesemwa katika ubalozi wa Iran mjini Algiers na Saeed Buhajeh, Spika wa Bunge la Algeria wakati akisaini daftari la kumbukumbu ya mashahidi waliouawa katika mashambulizi hayo ya Tehran, ambapo ametoa salamu za rambirambi kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, serikali na taifa la Iran kwa ujumla kufuatia hujuma hizo za kikatili.
Mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa Jumatano iliyopita na wanachama wa kundi la Daesh katika majengo ya Bunge la Iran na Haram ya Imam Khomeini (MA) mjini Tehran yalisababisha vifo vya watu 17 na kujeruhi wengine 52.
Spika wa Bunge la Algeria amebainisha kuwa, Tehran na Algiers zina historia ya jadi na pana ya kupambana na ugaidi na misimamo ya kuchupa mipaka na kusisitiza kuwa, pande mbili hizo ziko tayari kuimarisha ushirikiano wao katika kila uga ukiwemo ushirikiano wa kibunge.
Kwa upande wake, Reza Ameri, Balozi wa Iran mjini Algiers amesema Jamhuri ya Kiislamu imekuwa mhanga wa miaka mingi wa mashambulizi ya kigaidi na kusisitiza kuwa hujuma za hivi karibuni za Tehran kama za huko nyuma, katu hazitoitoa nchi hii katika njia yake.
Kadhalika ameongeza kuwa, Iran na Algeria ni nchi mbili za kimapinduzi na zenye ukwasi mkubwa wa thamani za kimapinduzi na kwamba moyo wa mapmbano na subra wa Wairani utapelekea vitendo hivyo vya kigaidi dhidi yake viimarishe umoja na mshikamano wao sanjari na kuwatumbukia nyongo maadui wa taifa hili.