Ufaransa na malengo ya kisiasa na kiuchumi katika eneo la Sahel, Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31272-ufaransa_na_malengo_ya_kisiasa_na_kiuchumi_katika_eneo_la_sahel_afrika
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliwasili jana mjini Bamako, mji mkuu wa Mali kwa lengo la kushiriki katika kikao kilichopewa anwani ya 'Kundi la Nchi Tano za Sahel' na katika fremu ya kuundwa kikosi cha kijeshi cha nchi za eneo hilo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jul 03, 2017 02:32 UTC
  • Ufaransa na malengo ya kisiasa na kiuchumi katika eneo la Sahel, Afrika

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliwasili jana mjini Bamako, mji mkuu wa Mali kwa lengo la kushiriki katika kikao kilichopewa anwani ya 'Kundi la Nchi Tano za Sahel' na katika fremu ya kuundwa kikosi cha kijeshi cha nchi za eneo hilo.

Nchi zinazokusudiwa za eneo la Sahel ni Chad, Niger, Burkina Faso, Mali na Mauritania, ambazo kwa pendekezo na uungaji mkono wa Paris, zimekusudia kuunda kikosi kitakachokuwa na askari 5000 wakiwemo askari jeshi, polisi na raia kwa lengo la kukabiliana na harakati za kigaidi na makundi yenye kufurutu ada katika eneo hilo. Katika mkondo huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia wiki iliyopita lilipasisha muswada wa kukubaliana na pendekezo la Ufaransa la kuundwa kikosi hicho cha majeshi ya nchi tano zilizotajwa. François Delattre, mwakilishi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, azimio hilo ni ujumbe imara kwamba, katika kupambana na ugaidi ndani ya eneo hilo la Sahel, wanachama wa umoja huo wameungana na kuonyesha kwamba, sasa jukumu hilo ni lina umuhimu mkubwa kuliko wakati mwingine wowote.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alipowasili Mali katika safari yake ya kwanza

Ni muda sasa ambapo harakati za makundi ya kigaidi katika bara la Afrika zimekuwa zikihatarisha usalama na amani katika maeneo tofauti ya bara hilo, kiasi kwamba baadhi ya nchi za Kiafrika zimegeuka na kuwa ngome za kuendeshea harakati za kigaidi za magenge hayo. Mapigano na vita vya ndani vinavyosababishwa na tofauti za ndani za kisiasa, kikaumu, kikabila na kidini, vinatajwa kuwa chanzo cha nchi nyingi kukumbwa na wimbi la ugaidi. Hali hiyo ndio inayoshuhudiwa pia nchini Mali ambapo makundi ya kigaidi ya kaskazini mwa nchi hiyo yanashirikiana na makundi yanayotaka kujitenga eneo hilo. Kupanuka kwa harakati za kigaidi na ongezeko la makundi yenye kufurutu ada katika eneo hilo kwa upande mmoja na kadhalika kuongezeka kwa mashambulizi ya kigaidi katika nchi za Ulaya hususan Ufaransa kwa upande wa pili, vimezidisha umuhimu wa mapambano dhidi ya ugaidi hususan kwa viongozi wa Ulaya.

Wanamgambo wanaohatarisha usalama eneo la Sahel

Kwa sasa serikali za nchi za Ulaya ikiwemo Ufaransa, zinafanya jitihada sambamba na kujidhaminia usalama, ziimarisha pia uepo wao katika nchi za Kiafrika ili kwa njia hiyo ziweze kuzinyonya kisiasa na kiuchumi nchi za bara hilo. Ni kwa sababu hiyo ndio maana katika safari yake nchini Mali inayofanyika siku chache tu baada ya kuapishwa, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameahidi kulibakisha jeshi la nchi yake katika eneo la Sahel huko Afrika. Kadhalika Macron ametangaza kuwa, operesheni za kijeshi za kuzuia kuhuishwa tena makundi yenye kufurutu ada katika eneo hilo, ni lazima ziongezwe nguvu.

Kuendelea kuwepo askari wa Ufaransa katika eneo la Sahel barani Afrika kunajiri katika hali ambayo, gharama kubwa zinazotumiwa kwa ajili ya askari hao hasa kwa kuzingatia hali mbaya ya kiuchumi na kisiasa inayoshuhudiwa hivi sasa nchini Ufaransa, zimeisababishia changamoto kubwa serikali ya Paris.

Magaidi hao

Kufuatia hali hiyo, hivi sasa Rais Emmanuel Macron anajitahidi kuhakikisha mzigo wa gharama za kuwepo askari wa nchi yake katika eneo hilo unabebwa na nchi nyingine, suala ambalo linaonekana kuwa kikwazo kwa serikali ya Paris. Hii ni kwa kuwa, kwa upande mmoja, Umoja wa Mataifa umetaka muda wa miezi miwili zaidi kwa ajili ya kukusanya bajeti ya kundwa kikosi cha nchi tano katika eneo la Sahel, na kwa upande mwingine nchi ya Chad ambayo inachangia sehemu kubwa ya askari katika kikosi hicho tayari imetishia kwamba, iwapo haitadhaminiwa bajeti ya mahitaji yake, serikali ya N'Djamena haitachangia askari katika kikosi hicho.

Inafaa kuashiria kuwa, eneo la Sahel linahesabiwa kuwa kati ya maeneo nyeti na yenye machafuko sana na ni kwa msingi huo mbali na kushuhudia harakati za makundi ya kigaidi na yenye kufurutu ada, kunashuhudiwa pia ushindani wa kimataifa na kikanda kutokana na kuwa na utajiri wa madini na akiba ya mafuta.

Ukweli ni kwamba kudhibiti eneo hilo kunaweza kuwa ufunguo wa kudhibiti maeneo mengine ya Afrika na ni kwa sababu hiyo ndio maana sambamba na kupanua siasa zake, Ufaransa inafanya juhudi kubwa ili iweze kuwabakisha askari wake katika eneo hilo kama hatua moja mbele ya kuweza kudhibiti maeneo mengine ya Afrika.