Wapinzani wa serikali ya Misri wanapanga kumuondoa madarakani al Sisi
Mamia ya wapinzani wa serikali ya Misri walioko nje ya nchi wamenzisha kampeni ya kuunga mkono harakati ya kumuondoa madarakani Rais wa sasa wa nchi hiyo, Abdul Fattah al Sisi.
Ripoti zinasema, sambamba na kumbukumbu ya kutimia mwaka wa nne tangu jeshi la Misri lifanye mapinduzi dhidi ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Mohamed Morsi, wapinzani 900 wa serikali ya Cairo wanaoishi nje ya nchi wameanzisha kampeni ya kuiondoa madarakani serikali ya Abdul Fattah al Sisi, kurejeshwa serikali halali na kumuunga mkono Morsi.
Taarifa iliyotolewa na kundi hilo imesema kuwa, takwa la kuondolewa madarakani serikali ya al Sisi si la wasomi na watu mashuhuri walioanzisha kampeni hiyo pekee, bali ni takwa halali la matabaka yote ya raia wa Misri.
Wakati huo huo Jumuiya ya Kiarabu ya Haki za Binadamu yenye makao yake mjini London nchini Uingereza imetoa ripoti kuhusu jinai na ukandamizaji mkubwa uliofanywa na serikali ya Jenerali Abdul Fattah al Sisi katika kipindi cha miaka minne iliyopita na kusisitiza kuwa, hali mbaya ya haki za binadamu nchini Misri bado haijabadilika.
Ripoti hiyo imesema kuwa, katika kipindi hicho cha miaka minne serikali ya al Sisi imeua watu 2,934 kinyume cha sheria.
Mwaka 2013 Jenerali mstaafu Abdul Fattah al Sisi aliongoza mapinduzi yaliyoiondoa madarakani serikali ya kwanza ya kidemokrasia nchini humo na hadi sasa inamshikilia korokoroni rais wa serikali hiyo, Mohamed Morsi.