Genge lenye mfungamano na Daesh laangamizwa Tunisia
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imetangaza kuwa imegundua na kuliangamiza genge moja lenye mfungamano na kundi la kigaidi ma kitakfiri la Daesh katika eneo la Zaafaran katikati mwa nchi hiyo.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imetangaza kuwa genge hilo lenye mfungamano na Daesh limegunduliwa na kuangamizwa kufuatia upelelezi wa kiintelijinsia uliofanywa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imeongeza kuwa magaidi wa kitakfiri zaidi ya 30 wametiwa mbaroni kwenye oparesheni hiyo. Vikosi vya usalama vya Tunisia vinaendesha mapambano dhidi ya makundi ya wanamgambo ambayo katika mwaka mmoja uliopita yamekuwa yakishambulia vituo vya jeshi na polisi wa doria katika maeneo ya mbali ya mpakani mwa nchi hiyo.
Itakumbukwa kuwa kundi la kigaidi la Daesh lilihusika katika mashambulizi matatu makubwa mwaka uliopita katika maeneo ya utalii nchini humo. Watu 60 wengi wao wakiwa ni raia wa nchi ajinabi waliuawa kwenye mashambulizi hayo.