Msomi wa Misri: Uislamu sio dini ya kufurutu ada na utumiaji mabavu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31870-msomi_wa_misri_uislamu_sio_dini_ya_kufurutu_ada_na_utumiaji_mabavu
Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Dini katika Bunge la Misri amesema kuwa, Uislamu sio dini ya kufurutu ada, aasubi na utumiaji mabavu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 17, 2017 04:25 UTC
  • Msomi wa Misri: Uislamu sio dini ya kufurutu ada na utumiaji mabavu

Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Dini katika Bunge la Misri amesema kuwa, Uislamu sio dini ya kufurutu ada, aasubi na utumiaji mabavu.

Osama al-Abd, Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Dini katika Bunge la Misri ameashiria matukio ya hivi karibuni ya kigaidi katika nchi hiyo na kusema kuwa, watu wenye misimamo ya kufurutru ada ndio wanaobeba dhima ya matukio ya kigaidi ya hivi karibuni katika nchi hiyo. 

Ameongeza kuwa, kuna haja ya kuongezwa juhudi za kieneo na kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi na kuutokomeza. Aidha Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Dini katika Bunge la Misri ametaka kuchukuliwa hatua za kukabiliana na watu wanaoeneza mbinu potofu kwa kutumia mgongo wa dini.

Vikosi vya usalama vya Misri vikiwa Sinai

Katika shambulio la hivi karibuni kabisa nchini Misri, polisi wasiopungua 5 waliuawa katika jimbo la Sinai na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la magaidi wa Daesh katika jimbo hilo.

Ikumbukwe kuwa, mwanzoni mwa mwezi huu wanajeshi wasiopungua 23 wa Misri waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya bomu katika vituo vya upekuzi kaskazini mwa jimbo la Sinai. 

Mkoa wa Sinai huko Misri ni moja ya ngome kuu za tawi la wanamgambo wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh ambalo linaendesha harakati zake katika eneo hilo.