Wanajeshi watano wauawa kaskazini mwa Misri
Wanajeshi wasiopungua watano wa serikali ya Misri wameuawa katika mripuko wa bomu uliotokea kwenye mkoa wa Sinai Kaskazini.
Duru rasmi za Misiri zimetangaza kuwa, mripuko huo ulitokea jana Jumatatu ndani ya gari la deraya katika mji wa al Arish wa mkoa wa Sinai Kaskazini na kuua wanajeshi watano wa Misri.
Kwa miaka kadhaa sasa, mkoa huo wa kaskazini mwa Misri umekuwa uwanja wa mashambulizi ya makundi yenye silaha. Kundi hatari zaidi ni lilel linalojiita Ansar Bait al Muqaddas ambalo limetangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi la wakufurishaji yaani Daesh.
Siku chache zilizopita, ndege za kivita za jeshi la Misri lilishambulia maficho kadhaa ya makundi ya kigaidi katika mkoa wa Sinai Kaskazini.
Juzi Jumapili, jeshi la Misri lilitangaza habari ya kuuawa magaidi watatu wakufurishaji katikati ya Rasi ya Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo.
Shirika la habari la Ufaransa lililinukuu taarifa ya jeshi la Misri ikisema kuwa, askari wa jeshi hilo wamefanikiwa kuangamiza magaidi watatu na kumtia mbaroni mwengine mmoja.
Taarifa ya jeshi hilo ilieongeza kuwa, askari wa jeshi hilo wameshambulia maficho ya magaidi katika operesheni ya kuyasafisha maeneo hayo na uwepo wa magaidi wenye misimamo mikali na kufanikiwa kuteketeza maghala matano ya silaha za magaidi hao.
Hivi sasa serikali ya Misri imeshadidisha mashambulizi yake kwa shabaha ya kuwafuta kabisa magaidi wenye misimamo mikali ambao wana maficho yao katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri.