Watu 7 wauawa katika shambulio la bomu Sinai, Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32250-watu_7_wauawa_katika_shambulio_la_bomu_sinai_misri
Raia 7 wakiwemo watoto wawili wameuawa katika shambulio la bomu la kutegwa garini katika Peninsula ya Sinai, kaskazini mwa Misri.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 25, 2017 09:51 UTC
  • Watu 7 wauawa katika shambulio la bomu Sinai, Misri

Raia 7 wakiwemo watoto wawili wameuawa katika shambulio la bomu la kutegwa garini katika Peninsula ya Sinai, kaskazini mwa Misri.

Msemaji wa jeshi la Misri amesema gari lililokuwa limetegwa bomu liliripuka katika kituo cha upekuzi karibu na mji wa al-Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini jana Jumatatu, ambapo mbali na mauaji hayo, watu wengine kadhaa walijeruhiwa.

Amesema watu wanne waliokuwa wamejizatiti kwa bunduki walikuwa kwenye gari hilo lililoripuka. Hakuna kundi lililotangaza kufanya hujuma hiyo ya jana Jumatatu.

Wiki iliyopita, wanajeshi wasiopungua watano wa Misri waliuawa katika mripuko mwingine wa bomu lililotegwa ndani ya gari la deraya, katika mji huo wa al-Arish, mkoa wa Sinai Kaskazini.

Magaidi wakufurishaji wa eneo la Sinai wakifanya jinai zao

Mkoa huo wa kaskazini mwa Misri umekuwa uwanja wa mashambulizi ya makundi yenye silaha. Kundi hatari zaidi ni lile linalojiita Ansar Bait al Muqaddas ambalo limetangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).

Hivi sasa serikali ya Misri imeshadidisha mashambulizi yake kwa shabaha ya kuwafuta kabisa magaidi wenye misimamo mikali ambao wana maficho yao katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo.