UN: Tuna wasiwasi CAR itatumbukia tena katika machafuko makubwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32336-un_tuna_wasiwasi_car_itatumbukia_tena_katika_machafuko_makubwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa, yumkini Jamhuri ya Afrika ya Kati ikajikuta imetumbukia tena katika mgogoro mpana na machafuko makubwa ambayo yatavuruga jitihada za kurejesha amani na uthabiti katika nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 27, 2017 10:45 UTC
  • UN: Tuna wasiwasi CAR itatumbukia tena katika machafuko makubwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa, yumkini Jamhuri ya Afrika ya Kati ikajikuta imetumbukia tena katika mgogoro mpana na machafuko makubwa ambayo yatavuruga jitihada za kurejesha amani na uthabiti katika nchi hiyo.

Antonio Guterres amesema iwapo wimbi jipya la mapigano na harakati za magenge ya waasi hazitasitishwa haraka iwezekanavyo, basi kuna uwezekano mkubwa nchi hiyo ikashuhudia machafuko ya umwagikaji wa damu kama huko nyuma.

Sambamba na kulaani mauaji ya maafisa wawili wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) hivi karibuni, Guterres amesema ni jambo la kutisha kuona genge la waasi wa Anti-Balaka ambalo mwaka huu pekee limeua askari tisa wa kofia buluu wa UN, linaendeleza mauaji ya kutisha huku wanachama wake wakidhani kuwa hawatawajibishwa.

Jumanne iliyopita, kundi la kigaidi la Kikristo la Anti-Balaka liliua wanajeshi wawili raia wa Morocco wa MINUSCA katika mji wa Bangassou, yapata kilomita 700 mashariki mwa mji mkuu Bangui.

Baadhi ya wanachama wa wapiganaji wa Anti-Balaka

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka pande zote husika kusitisha mapigano na kuchukua hatua za makusudi ili kuhakikisha kuwa usalama mdogo unaoshuhudiwa nchini humo hautoweki na hali kuzidi kuwa mbaya.

Mwezi Mei mwaka huu, watu 115 aghalabu yao wakiwa wafuasi wa dini ya Kiislamu waliuawa na wapiganaji wa Anti-Balaka, katika mji wa Bangassou, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.