Wanaharakati watahadharisha kushadidi machafuko mashariki mwa Sudan
Wanaharakati za asasi za kiraia nchini Sudan wametahadharisha kuhusiana na uwezekano wa kushadidi machafuko na ukosefu wa amani katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Kundi la Sudan Democracy First Group imeeleza kuwa, matatizo na sababu zilizopelekea kushadidi mapigano mashariki mwa Sudan bado hayajapatiwa ufumbuzi hivyo kuna uwezako wa kushadidi tena hali ya ukosefu wa amani katika maeneo hayo.
Taarifa hiyo imesema kuwa, wakati wowote kuanzia sasa inawezekana maeneo ya mashariki mwa Sudan yakakumbwa na mgogoro uliowahi kutokea katika maeneo hayo miaka ya nyuma.
Aidha Kundi la Sudan Democracy First Group limesema kuwa, serikali ya Khartoum ndio inayobeba dhima ya kuongezeka ubaguzi wa kijamii mashariki mwa Sudan ambao umepelekea maeneo ya nchi hiyo kukumbwa na hali mbaya ya mgogoro.
Kundi hilo limetoa wito wa kuongezwa juhudui maradufuza kitaifa kwa shabaha ya kuyaepusha maeneo hayo ya mashariki mwa Sudan yasije yakarejea tena katika hali ya wakati wa vita vilivyokuwa na uharibifu.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Sudan imeendelea kuwa na mivutano na jirani yake sudan Kusini.
Mwanzoni mwa mwezi huu viongozi wa Sudan na Sudan Kusini walikubaliana kuhusu mpango wa usuluhishi wa Umoja wa Afrika ili kukomesha uhasama na mzozo kati yao na kuanza tena mazungumzo ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kiusalama na kijeshi kati ya nchi mbili hizo.