Dakta Larijani: Kuna fursa nyingi za kushirikiana Iran na Uganda
Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, Iran na Uganda zina vyanzo vingi vya utajiri na kwamba, kuna fursa nyingi za kushirikiana Tehran na Kampala.
Dakta Ali Larijani amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Jenerali Moses Ali, Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu wa Uganda na kuitaja Uganda na wananchi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwamba, ni marafiki wa karibu wa Iran.
Dakta Larijani amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha hatua za kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Tehran na Kampala.
Kwa upande wake Jenerali Moses Ali, Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu wa Uganda sambamba na kusisitiza kwamba, Kampala ina azma na nia ya kukuza ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema wazi kwamba, Iran ni taifa muhimu ulimwenguni ambalo lina utamaduni na ustaarabu mkongwe na wenye thamani kubwa.
Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu wa Uganda ameongeza kuwa, nchi yake inataka kustafidi na tajiriba na uzoefu ilionao Iran katika nyanja mbalimbali zikiwemo za sekta za mafuta na petrokemikali.
Moses Ali, Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu wa Uganda yuko hapa mjini Tehran kuhudhuria sherehe ya kuapishwa Rais Hassan Rouhani, itakayofanyika kesho Jumamosi katika ukumbi wa Bunge la Iran, sherehe ambayo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi na wawakilishi wa karibu nchi mia moja duniani.