Umoja wa Mataifa waonya kuhusu dalili za mauaji ya kimbari CAR
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea mauji ya kimbari huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Stephen O’Brien, Mshirikishi wa UN katika masuala ya masuala ya haki za binadamu na misaada ya dharura amesema kuzuka tena mapigano huko CAR ni dalili tosha kuwa nchi hiyo ya Kiafrika ipo katika ncha ya kutumbukia katika mauaji ya kimbari.
O'Brien ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyasema hayo jana Jumatatu, baada ya kutamatisha safari yake huko CAR na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ameongeza kuwa, watu zaidi ya 180,000 wamefurushwa katika makazi yao nchini humo mwaka huu, na kupelekea idadi ya wakimbizi wa nchi hiyo ya Kiafrika kupindukia nusu milioni hasi sasa.
Wiki iliyopita, Jean-Pierre Lacroix, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kusimamia amani alionyesha wasi wasi wake mkubwa kutokana na kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu na machafuko nchini CAR.
Mwezi uliopita, ripoti iliyotolewa na Human Rights Watch ilisema kuwa, makundi ya wanamgambo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati yalifanya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu katika kipindi cha kati ya mwaka 2014 na 2017. Ripoti hiyo ya HRW imesajili mauaji ya watu 566 na kusisitiza kuwa hiyo ni sehemu ndogo ya jinai zilizofanywa na magenge ya wanamgambo wanaobeba silaha nchini humo.