Misri yalalamikia hatua ya Marekani ya kuikatia misaada
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33572-misri_yalalamikia_hatua_ya_marekani_ya_kuikatia_misaada
Serikali ya Misri imekosoa vikali hatua ya Marekani ya kuikatia misaada nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kutahadharisha juu ya taathira hasi inayoikodolea macho Washington kutokana na kitendo chake hicho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 24, 2017 09:22 UTC
  • Misri yalalamikia hatua ya Marekani ya kuikatia misaada

Serikali ya Misri imekosoa vikali hatua ya Marekani ya kuikatia misaada nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kutahadharisha juu ya taathira hasi inayoikodolea macho Washington kutokana na kitendo chake hicho.

Viongozi wa Misri wametoa lalama hizo mjini Cairo katika mkutano wao na ujumbe wa ngazi ya juu ya Marekani unaoongozwa na Jared Kushner, mshauri wa Ikulu ya White House, ulioko katika nchi hiyo ya Kiarabu kwa ajili ya kile kinachotajwa kuwa mchakato wa amani wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Israel na Palestina.

Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri aliyekutana na viongozi hao wa Marekani amesema uamuzi huo wa Marekani umechukuliwa katika anga isiyo ya uadilifu na kwamba yumkini ukawa na madhara makubwa katika uhusiano wa muda mrefu wa Cairo na Washington.

Jumanne iliyopita, Washington ilitangaza kuikatia Misri misaada ya dola milioni 96 za Marekani, kwa madai kuwa serikali ya Cairo ina rekodi mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu. Kadhalika US imeicheleweshea Misri msaada wa kijeshi wa dola milioni 195.

Trump na al-Sisi wakipeana mikono

Hatua hiyo ya Marekani imeishangaza Misri ambayo ilikuwa na wingi wa matumaini ya kuwa na uhusiano mzuri wa pande mbili na Washington, haswa baada ya Rais Donald Trump kuahidi kwamba atahuisha uhusiaono huo uliokuwa umeingia doa wakati wa utawala wa Barack Obama.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ikiwemo Amnesty International yanasema kuwa, mamia ya watu wameuawa na maafisa usalama nchini Misri tangu Rais Abdul Fattah al-Sisi alipoigia madarakani Julai 2013, mbali na zaidi ya 20,000 kuzuiliwa kinyume cha sheria.