Sep 08, 2017 06:52 UTC
  • Utawala mbovu, chanzo cha vijana kuwa na misimamo mikali Afrika

Vijana wa Afrika wanajiunga na makundi yenye misimamo mikali kutokana na sababu kadhaa ikiwemo kupuuzwa, kunyimwa fursa pamoja na ukosefu wa utawala bora.

Hayo yamedokezwa na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo, UNDP kanda ya Afrika Abdoulaye Mar Dieye alipowasilisha matokeo ya utafiti wake katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.

Abdoulaye Mar Dieye ameongeza kuwa, ijapokuwa dini inaweza kuonekana kuwa kichocheo cha mara kwa mara cha  watu kujiunga na makundi ya kigaidi yenye misimamo mikali, lakini kiwango cha uelewa wa kidini ni kidogo sana au hakipo kabisa miongoni mwa wale waliojiunga na vikundi hivyo.

Aidha afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema changamoto kwa mwelekeo wa sasa wa chuki dhidi ya Waislamu imetokana na kuenea misimamo mikali ya kidini.

Kwa mantiki hiyo utafiti huo unapendekeza kuchukuliwa hatua stahili za kuepusha vijana wa Afrika kuingia kwenye vikundi vyenye misimamo mikali ikiwemo kuweka tawala ambazo ni jumuishi na shirikishi hasa katika ngazi ya jamii. Barani Afrika hivi sasa makundi makubwa zaidi ya wenye misimamo mikali ya kidini ni pamoja na kundi la kigaidi na la ukufurishaji la al Shabab lenye makao yake Somalia ambalo pia hufanya mashambulizi ya mara kwa mara katika nchi jirani ya Kenya. Kundi jingine ni lile la Boko Haram la nchini Nigeria ambalo nalo pia hufanya mashamabulizi katika nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger.

Tags