UN yataka kuongezwa askari wa kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kimetoa mwito wa kutumwa katika nchi hiyo mamia ya askari zaidi ili kujaza pengo lililoachwa baada ya Uganda kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, barua ya siri kutoka kwa Parfait Onanga-Anyanga, Mkuu wa kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa imeitaka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kusimamia Operesheni za Kulinda Amani yenye makao makuu yake mjini New York kutuma wanajeshi 750 katika nchi hiyo ya Kiafrika.
Barua hiyo imesema kuwa, wanajeshi hao wapya wanahitajika kusini mashariki mwa nchi baada ya Uganda kuwarejesha nyumbani wanajeshi wapatao 500 wa UPDF mwaka huu, huku Marekani pia ikiwaondoa katika eneo hilo makumi ya askari wake wa Kikosi Maalumu.
Kwa sasa kuna wanajeshi 10,750 wa Kofia Buluu na askari polisi 2,080 wa UN nchi humo na iwapo ombi la Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati litakubaliwa, basi nchi hiyo itakuwa na jumla ya maafisa usalama wapatao 13,500 wa umoja huo.
Haya yanajiri siku chache baada ya watu 25 kuuawa katika mapigano mapya huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, sambamba na kupigwa kalamu nyekundu Levy Yakete, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo kutokana na ongezeko la machafuko.