HRW: Ubakaji unatumika kama silaha ya vita Jamhuri ya Afrika ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35257-hrw_ubakaji_unatumika_kama_silaha_ya_vita_jamhuri_ya_afrika_ya_kati
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema ubakaji na dhulma za kijinsia zinatumiwa kama mbinu ya vita na magenge ya waasi wanaobeba silaha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Oct 05, 2017 10:26 UTC
  • HRW: Ubakaji unatumika kama silaha ya vita Jamhuri ya Afrika ya Kati

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema ubakaji na dhulma za kijinsia zinatumiwa kama mbinu ya vita na magenge ya waasi wanaobeba silaha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Ripoti ya HRW iliyotolewa leo Alkhamisi imeonyesha kuwa, kumenakiliwa kesi 305 za ubakaji na utumwa wa ngono miongoni mwa wanawake na wasichana 296, kati ya mwaka 2013 na katikati ya mwaka huu 2017 nchini humo.

Ripoti ya shirika hilo lenye makao yake mjini New York imesisitiza kuwa, yumkini idadi ya wanawake na mabinti waliobakwa ikawa ya juu zaidi, kwani baadhi ya waathiriwa wa jinai hizo dhidi ya binadamu walikataa kuhojiwa wala kuzungumzia suala hilo wakihofia unyanyapaa.

Waasi wa kundi la Kikristo la Anti-Balaka la CAR

Hivi karibuni, Umoja wa Mataifa ulitahadharisha kuhusiana na kuweko ishara za kutokea mauaji ya kimbari katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, licha ya uwepo wa askari elfu 10 wa kusimamia amani wa UN. 

Mapigano kati ya makundi hasimu ya wabeba silaha katika miezi ya hivi karibuni nchini humo yamesababisha mamia ya raia kuuawa na maelfu ya wengine kuwa wakimbizi. Watu milioni 2.4 wa CAR wanahitajia misaada ya dharura. 

Mapigano ya Jamhuri ya Afrika ya Kati yalianza Machi mwaka 2003 baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo François Bozizé.