Serikali ya Sudan yafunga mipaka kwa ajili ya kukusanya silaha
Serikali ya Sudan imefunga mipaka ya nchi hiyo katika utekelezaji wa mpango wa kukusanya silaha na imewataka raia wa nchi hiyo kuisaidia katika mchakato huo.
Makamu wa Rais wa Sudan, Hasabo Mohammed Abdul Rahman amesema kuwa, kuwepo silaha kwa wingi nchini humo kumechochea vita na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na kwamba, kwa kutilia maanani uhalifu unaofanyika dhidi ya raia, serikali ya Khartoum imechukua hatua za kuzuia harakati za kuingizwa silaha zaidi nchini humo.
Tathmini zinaonesha kuwa, karibu silaha milioni mbili zimezagaa kati ya raia wa Sudan na kwamba laki mbili kati ya silaha hizo ziko kwenye eneo lenye machafuko la Darfur.
Mapigano ya ndani nchini Sudan yalishika kasi mwaka 2003 baada ya watu wa eneo la magharibi mwa nchi hiyo la Darfur kuituhumu serikali ya Khartoum kwamba inawabagua.
Hadi sasa zaidi ya raia laki tatu wameuawa na karibu milioni mbili wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na mapigano hayo.