Oct 19, 2017 14:03 UTC
  • Boko Haram washambulia msafara wa wanajeshi Nigeria

Wanajeshi watatu wa Nigeria wameuawa baada ya kushambuliwa na genge la kigaidi na la ukufurishaji la Boko Haram.

Shambulio hilo la jana limetokea mjini Damboa na ni la pili kufanywa na kundi hilo dhidi ya wanajeshi wa Nigeria katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Nigeria amesema kuwa, wanajeshi hao watatu wameuawa baada ya kundi la kigaidi la Boko Haram kushambulia msafara wa wanajeshi katika eneo lililoko baina ya Damboa na Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno ambalo wakati fulani lilikuwa ni ngome ya Boko Haram.

Wanajeshi wa Nigeria wakilinda usalama katika jimbo la Borno

 

Siku ya Ijumaa, mwanajeshi mmoja wa Nigeria aliuawa na wengine tisa kujeruhiwa baada ya wanamgambo wakufurishaji wa kundi la Boko Haram kuvamia kambi ya kijeshi katika mji wa Marte ulioko karibu na fukwe za Ziwa Chad. Wanamgambo hao walipora silaha kwenye kambi hiyo na kuondoka nazo.

Afisa huyo mwandamizi wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wamejibu mashambulizi hayo, lakini wamepoteza wanajeshi watatu.

Magari yanayoingia na kutoka mjini Maiduguri yanahitajia kusindikizwa na jeshi kutokana na kushambuliwa mara kwa mara na magaidi wa Boko Haram.

Tarehe 12 mwezi huu wa Oktoba, watu wengine watano waliuawa baada ya gaidi mmoja kujiripua kwa bomu katika kijiji cha Belbelu, karibu na Kayamla, katika eneo la Konduga la jimbo lenye usalama mdogo la Borno, la kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Tags