WHO: Watu 94 wameaga dunia kwa ugonjwa wa tauni nchini Madagascar
Idadi ya vifo vilivyosababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa tauni nchini Madagascar hadi sasa vimefikia 94 huku kesi nyingine za maambukizi ya ugonjwa huo zikiwa zaidi ya 1,100.
Maafisa katika taifa hilo maskini linalopatikana katika Bahari ya Hindi mapema wiki hii waliripoti habari ya kuaga dunia watu 74 na kuambukizwa wengine 805. Ibrahima Soce Fall, Mkurugenzi wa WHO barani Afrika amesema kuwa kesi 300 za maambukizo ya tauni zimethibitishwa kimaabara kati ya kesi 1153 zilizokuwa zikishukiwa.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, Fall amesema kuwa, Shirika la Afya Duniani tayari limetuma dozi milioni 1.3 za dawa za kiuavijasumu kwa ajili ya kutibu wagonjwa 5000 na kuwakinga wengine laki moja ambao wapo katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo. Amesema maambukizi ya ugonjwa huo wa tauni yanaenea kwa kasi kubwa nchini Madagascar na kwamba inatazamiwa kuwa kutaripotiwa kesi zaidi za maambukizi ya homa hiyo.
Madagascar imekuwa ikiathiriwa na mlipuko wa tauni karibu kila mwaka tangu mwaka 1980 katika kipindi maalumu kati ya mwezi Septemba na Aprili.