Oct 20, 2017 16:48 UTC
  • Uganda yakumbwa tena na homa ya Marburg

Uganda imethibitisha kufariki dunia mtu mmoja kwa homa inayoenezwa na kirusi cha Marburg, homa ambayo huambatana na kuvuja damu sawa kabisa na homa ya Ebola. Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya wa nchi hiyo.

Jane Ruth Aceng ameueleza mkutano wa waandishi wa habari kwamba kesi hiyo ya mambukizo ya homa ya Marburg imethibitishwa baada ya kufanyika chunguzi kadhaa. Nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika mara ya mwisho kuathiriwa na mlipuko wa homa ya Marburg ilikuwa mwaka 2014. Virusi vya homa hiyo vinatoka katika familia moja sawa na vile vya homa ya Ebola iliyouwa maelfu ya watu magharibi mwa Afrika mwaka 2014.

Wafanyakazi wa afya wakiwapima raia kama wameambukizwa homa ya ebola 

Waziri wa Afya wa Uganda ameongeza kuwa, mhanga wa homa hiyo ya Marburg ametajwa kuwa mwanamke aliyekuwa na umri miaka 50 ambaye aliaga dunia tarehe 11 mwezi huu katika hospitali moja mashariki mwa Uganda baada ya kuwa na dalili na viasharia vilivyosadikiwa kuwa ni homa ya kuvuja damu inayosababishwa na virusi.  

Imeelezwa kuwa mama huyo alikuwa akimhudumia kaka yake mwenye umri wa miaka 42 ambaye aliaga dunia Septemba 25 mwaka huu akiwa na dalili sawa na hizo. Mama huyo pia alishiriki katika kuandaa mwili wa kaka yake kwa ajili ya mazishi.

Mtu aliyeambukizwa homa ya Marburg huwa na dalili za maumivu ya kichwa, kutapika damu, maumivu ya misuli na kuvuja damu katika matundu kadhaa ya mwili.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kuwa limetuma maafisa nchini Uganda ili kuimarisha juhudi za kuzuia mlipuko wa homa hiyo. Uganda imeshawahi kukumbwa na milipuko ya homa ya Ebola na Marburg katika siku za nyuma, japokuwa milipuko hiyo kwa kiasi kikubwa ilizuiwa kuenea haraka na kusababisha maafa makubwa.

Tags