Wanamgambo wa Hasm waua maafisa wasiopungua 30 wa polisi nchini Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35842-wanamgambo_wa_hasm_waua_maafisa_wasiopungua_30_wa_polisi_nchini_misri
Mapigano yaliyotokea jana Ijumaa kati ya maafisa wa polisi na wanamgambo wa kundi la Hasm huko kusini mwa mji mkuu Cairo yamepelekea maafisa wasiopungua 30 wa polisi kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 21, 2017 00:50 UTC
  • Wanamgambo wa Hasm nchini Misri
    Wanamgambo wa Hasm nchini Misri

Mapigano yaliyotokea jana Ijumaa kati ya maafisa wa polisi na wanamgambo wa kundi la Hasm huko kusini mwa mji mkuu Cairo yamepelekea maafisa wasiopungua 30 wa polisi kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Duru za usalama na za hospitali zimethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, wanajeshi na polisi wasiopungua 30 wameuawa wakati walipovamia maficho ya wanamgambo wa Hasm kusini magharibi mwa Cairo, jana Ijumaa.

Mapigano hayo yametokea katika eneo la Bahariya, yapata kilomia 135 kusini magharibi mwa Cairo, baada ya maafisa usalama wa Misri kupata taarifa za kuweko maficho ya wanamgambo hao kwenye eneo hilo.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imethibitisha habari ya kuuawa maafisa wa polisi na wanamgambo ingawa hata hivyo haikutoa maelezo zaidi.

Maafisa usalama wa Misri wakiwa kazini nchini Misri

 

Wakati huo huo askari 14 wa Misri wameuawa baada ya kuvamiwa na magaidi jana Ijumaa katika mkoa wa Giza wa magharibi mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Mtandao wa habari wa gazeti la Washington Post umetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, mbali na kuuawa askari hao 14, askari wengine wanane wa Misri wamejeruhiwa katika shambulizi hilo.

Hadi tunapokea habari hii hakuna kundi lolote lililokuwa limetangaza kuhusika na shambulio hilo hilo. Hata hivyo katika miezi ya hivi karibuni, kundi la Wilaya ya Sinai ambalo ni tawi la genge la kigaidi la Daesh nchini Misri limehusika na utegaji mwingi wa mabomu na mashambulizi ya kigaidi nchini humo.